Thursday, December 3, 2015

MHE. BALOZI WILSON MASILINGI AKUTANA NA MHE. BALOZI HUNAINAH ALMUGHEIRY WA OMAN WASHINGTON DCMhe. Wilson Masilingi, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Marekani akikaribishwa ofisini kwa Mhe. Balozi Hunaina Almugheiry, Balozi wa Oman nchini Marekani.

Mheshimiwa Wilson Masilingi, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Marekani alimtembelea Mhe. Hunainah AlMugheiry, Balozi wa Oman nchini Marekani, ofisini kwake Washington DC leo Alhamisi Desemba 3,2015. Katika mazungumzo Mhe. Balozi Masilingi aliambatana na Bw. Suleiman Ahmed Saleh, Afisa wa Ubalozi wa Tanzania Washington DC.

Mazungumzo kati ya Mhe. Balozi Masilingi na Mhe. Mugheiry yalilenga katika kuimarisha mahusiano kati ya nchi hizo mbili zenye mahusiano ya kidugu. Mhe. Balozi Mugheiry alifurahishwa na kuonana na Mhe. Masilingi na kubainisha kwamba Oman na Tanzania zina mahusiano ya kidamu na hivyo nchi hizo hazina budi kudumisha mahusiano hayo ya kihistoria. Mhe. Mugheiry alimweleza Balozi Masilingi kwamba amefarijika uchaguzi wa Tanzania ulikwisha salama na Tanzania kumpata mrithi wa Rais mpya Mhe. John Pombe Magufuli kufuatia kumaliza muda wake Rais aliyepita Mhe. Jakaya Kikwete.Aliongeza kwa kusema kwamba Oman na Tanzania zimekuwa na mashirikiano ya kiuchumi,kibiashara na kielimu na anaamini kwamba ujenzi wa bandari ya Bagamoyo na fursa za masomo ya juu zinazotolewa na Serikali ya Oman kwa wanafunzi wa Tanzania Bara na Visiwani ni vielelezo vya mahusiano hayo.

Kwa upande wake Mhe. Balozi Masilingi alifarijika sana kumsikia Mhe. Balozi Hunainah wa Oman akimwambia kwamba alizaliwa Dar-es-Salaam, Tanzania, na familia yake ina mizizi visiwani Zanzibar pia. Alimshukuru Balozi Hunainah kwa kumkaribisha ofisini kwake na kufahamiana naye na kuahidi kufanya naye kazi kwa karibu katika kuendeleza mahusiano baina ya nchi zao zenye mahusiano ya asili.

Mhe. Wilson Masilingi katika picha ya kumbukumbu na Mhe. Hunainah Almugheiry

1 comment: